27 Februari 2015 - 19:39
Wanajeshi watatu wauawa Ukraine

Wanajeshi watatu wameuliwa mashariki mwa Ukraine licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya jeshi na waasi.

Wanajeshi watatu wameuliwa mashariki mwa Ukraine licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya jeshi na waasi. Mauaji hayo yanapunguza matumaini ya kurejea kwa amani ya kudumu katika nchi ambayo imeshuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa mwaka mzima sasa. Hata hivyo, duru za kijeshi zinaripoti kwamba hali ni shwari katika maeneo mengi na kwamba wanajeshi wameanza kuondoa silaha nzito kwenye uwanja wa mapambano. Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko amesema hata kama wanajeshi na waasi wataweka silaha chini bado kuna kitisho kutoka kwa Urusi. Nchi za Magharibi zinamshutumu Rais Vladmir Putin kwa kuwatuma wanajeshi wake kupigana Ukraine na pia kuwapatia waasi silaha. Nalo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo linafanya mkutano wa dharura kuijadili hali ya usalama nchini Ukraine.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa unaonya kwamba hali nchini Syria inazidi kuwa mbaya baada ya nchi hiyo kushuhudia miaka minne ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Naibu Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Kyung-Wha Kang, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba mamilioni ya Wasyria wameathirika na matumizi ya nguvu, njaa na magonjwa. Baada ya waasi wa kundi la kigaidi la Daesh linalojiita Dola la Kiislamu kulazimisha baadhi ya ofisi za misaada ya kibinadamu zifungwe, zaidi ya watu 600,000 hawajapatiwa msaada wa chakula tangu Desemba mwaka jana. Naye Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, Antonio Gueterres, amesema nchi zinazopakana na Syria zinakabiliana na hali ngumu sana katika kuwahudumia wakimbizi wapatao milioni 4. Pamoja na hayo Gueterres amezitaka nchi za Ulaya zipokee wakimbizi wengi zaidi kutoka Syria.